Shambulizi linaloshukiwa kuwa la ndege zisizo na rubani za Marekani nchini Pakistani limemuua kiongozi mkuu wa kundi la al-Qaida ambaye anachukuliwa kuwa mmoja wa watu wenye nguvu zaidi wa kundi hilo katika eneo hilo.
Taarifa zilizochapishwa kwenye tovuti kadhaa za wanajihadi zinasema Khaled Bin Abdel Rahman al-Hussainan, kiongozi wa al-Qaida anayejulikana kama Abu Zaid, aliuawa siku ya Alhamisi au Ijumaa katika eneo la Kaskazini la Waziristan karibu na mpaka wa Afghanistan.
Vyanzo vya kikabila vinasema alikuwa amehamia mafichoni katika eneo hilo siku chache zilizopita.
Pakistan imerudia kukosoa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Marekani kama ukiukaji wa uhuru wake.
Wakati wa mkutano wa Alhamisi na balozi wa Marekani Richard Olson, Waziri Mkuu wa Pakistan Raja Pervez Ashraf alisema mashambulizi hayo hayana tija na akahimiza njia mbadala za kuwaangamiza magaidi. Maafisa wa Marekani wamesema mashambulizi hayo ni nyenzo muhimu katika kuwashinda wanamgambo.
Kando, Rais Asif Ali Zardari amemtembelea Malala Yousafzai, msichana wa Pakistan ambaye anaendelea kupata nafuu katika hospitali ya Uingereza baada ya kupigwa risasi kichwani kwa kuzungumza dhidi ya Taliban.
Mwandishi wa VOA anasema Zardari alitumia takriban nusu saa Jumamosi na kijana huyo na familia yake katika hospitali moja huko Birmingham. Pia, madaktari walimweleza rais wa Pakistani kuhusu hali yake.
Shirika la habari la Associated Press la Pakistan linasema Zardari atahudhuria hafla ya kimataifa mjini Paris siku ya Jumatatu kumuenzi Malala. Shirika la habari linasema pia atajadili masuala ya pande mbili na Rais wa Ufaransa Francois Hollande. Rais Zardari yuko katika ziara ambayo pia itampeleka Uturuki.
(VOA)


