Takriban Wasyria 2,000 waliokimbia ghasia katika nchi yao wamevuka na kuingia Uturuki katika muda wa saa 48 zilizopita, ikiwa ni ongezeko kubwa la idadi ya wakimbizi wa Syria ambao sasa wanapata hifadhi nchini Uturuki, wizara ya mambo ya nje ilisema Jumatano.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Uturuki Selçuk Ünal amesema wimbi la hivi punde la waliowasili nchini Uturuki limeleta jumla ya wakimbizi wa Syria waliopo Uturuki kufikia takriban 29,500, idadi kubwa zaidi ya wakimbizi nchini Uturuki kwa wakati mmoja tangu kuanza kwa machafuko yapata miezi 15 iliyopita.
Miongoni mwa wakimbizi wapya 2,000 walikuwa watu 43 waliojeruhiwa ambao wamelazwa hospitalini nchini Uturuki, Ünal alisema.
Uturuki imewapa hifadhi zaidi ya Wasyria 50,000 tangu Machi 2011 lakini maelfu wamerejea makwao nchini Syria.



